Home Travel Tanzania ni nchi bora ya kutalii duniani

Tanzania ni nchi bora ya kutalii duniani

889
0

Kwa nini Tanzania imekuwa namba moja kwenye mambo ya utalii duniani?

Kufuatia mkurupuko wa COVID-19, nchi nyingi zinazojishughulisha na masuala ya utalii zimekuwa na wakati mgumu wa kukabiliana na janga hili. Karantini imekuwa mojawapo ya njia za kupambana na janga hili, huku ikipelekea kusimamisha shughuli mbalimbali ikiwemo utalii.

Ukilinganisha na nchi zingine,  Tanzania imeweza kukabiliana na janga hili la COVID kwa kiasi kikubwa na kuruhusu kuendelea kwa shughuli zake za kiuchumi. Tangu mwezi Juni mwaka huu Tanzania imechukua tahadhari zote, baada ya kuwa na visa vichache sana vya ugonjwa huu.

Karibu nami nikuorodheshee mambo muhimu yanayohusu utalii, na kuifanya Tanzania kuwa vinara mwaka huu:

Nchi yenye majira mazuri ya hali ya hewa (Misimu) kwa mwaka mzima.

Ninasema hivi kwa sababu wengi hudhani kuwa endapo watahitaji kuona wanyama na kutembelea vivutio maalum wanavyovifahamu, kuwa vinawezekana kipindi cha majira ya kiangazi pekee. La hasha!

Nchi hii ina hali ya hewa rafiki na ambayo inaweza kukufanya utalii muda wowote, mwezi wowote, sehemu yoyote ile. Utakapopanga ratiba yako ya kufanya mapumziko au utalii Tanzania, hutokosa vya kufanya utalii ndani ya wiki husika.

Hali ya hewa ni ya kitropiki, yenye mvua za kawaida pamoja na joto la kawaida kwa binadamu. Unaweza kufika hadi maeneo magumu (remote areas) kwa msaada wa tour guides na wasaidizi wake.

Wanyamapori wanaohama kila mwaka na Baloon Safari

Kuhama kwa wanyama wa Serengeti, maarufu kama ‘The Serengeti Migration’ kulithibitishwa kama mojawapo ya maajabu saba ya asili ya Afrika mnamo tarehe 11 Feb 2013 jijini Arusha baada ya kupigiwa kura na wazoefu nguli duniani waliotambua jambo hili.

Serengeti migration hutokea kila mwaka kati ya Tanzania na Kenya. “Serengeti ni nyumbani kwa uhamiaji mkubwa zaidi duniani, na namna ya pekee ya kufaidi ajabu hili ni kulishuhudia ukiwa kwenye puto juu angani,” aliongezea Phillip Imler, rais wa maajabu saba ya asili.

Mwaka huu, usafiri huu wa angani kwa baloon pale Serengeti umepata tuzo ya kuwa usafiri bora wa watalii kwa mwaka 2020 kutoka TripAdvisor na pia TaNaPa kwa kuwatunuku kama vinara wa ‘hot air baloon operator’.

Kuwa na hifadhi nyingi za kitaifa

Tanzania ni nchi pekee yenye hifadhi nyingi zaidi za kitaifa kuliko zote duniani. Zipo zile za Kilwa, zenye historia ya Mreno na miji ya biashara za Kiswahili, ya zaidi ya miaka 500 iliyopita, kuna Selous Game reserve yenye aina maalum ya Tembo, Gombe Stream National park ambayo Jane Godall ameifanyia utafiti wa kina kwa Sokwe waliopo huko, Usangu, Njombe na zingine nyingi, zaidi ya 32.

Nchi yenye kilele cha mlima Kilimanjaro, Afrika

Mlima wa kipekee, wenye maajabu yake na unaotembelewa na watu mbalimbali maarufu duniani, una urefu wa mita 5895 kutoka usawa wa bahari. Kilele (cha Kibo, Mawenzi na Shira) hicho chenye saruji ya barafu yenye umbo la koni ni kivutio cha wapandaji milima wengi zaidi duniani.

Ukiachana na mlima huu, zipo sehemu mbalimbali za asili ambazo adventure ya kupanda milima huwa ya kupendeza na yenye changamoto mbalimbali, kulingana na uwezo wako. Ikiwemo ya milima ya Uluguru, Meru, Usambara, Rungwe na kadhalika.

Fukwe nzuri na za kuvutia

Hapa ninamaanisha fukwe nzuri na za kuvutia za kitalii zenye maji safi na salama, na pia zinazoruhusu kuogelea (snorkelling), kubarizi (sun bathing) na kadhalika, zikiwemo za ziwa Victoria, Kisiwa cha Mafia (Kilindoni, Utende), Jiji la Dar (Bongoyo na Mbudya), Mjini Mtwara (Makonde beach, Msimbati na nyinginezo). Pia zipo zile za starehe zilizopo visiwani Zanzibar zenye hoteli hadi ya nyota tano na kuendelea.

Nchi ya maziwa makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa)

Ziwa Victoria, ambalo ni chanzo cha mto Nile, chenye visiwa na mandhari za mawe za kuvutia, ni chanzo pia cha samaki aina ya Sato na Sangara, pia Piranha.

Kwa upande wa ziwa Tanganyika ambalo lina kina kirefu zaidi duniani, lina maji masafi ( 8% ya maji masafi duniani) na aina zaidi ya 500 ya jamii za samaki hupatikana hapa. Ziwa hili linasafisha kona za nchi za Burundi, Rwanda, Congo (DRC) na eneo kiduchu la Zambia.

Ziwa Nyasa nalo linaipakana Tanzania na Malawi na Msumbiji, na lina mamba na viboko wengi sana. Pia ni sehemu nzuri kwa ajili ya michezo ya majini na kuogelea (diving) yenye fukwe nzuri na za kuvutia (hasa kaskazini mwa ziwa, maarufu kama Matema).

Unapenda mlo wa asili na fresh?

Tanzania ina asili ya kuwa na aina nyingi za wanyama na mimea, na kupelekea upatikanaji wa urahisi wa aina nyingi za vyakula. Utakuta mboga za majani na nyama za mifugo mbalimbali,na hata wanyama wa mwituni kama swala, nyati, kiboko, n.k. ambazo ni nzuri na hazina madhara yoyote ya kiafya. Pia aina nyingi mno za samaki wa baharini wakiwemo lobsters, kaa, pweza, ngisi, taa na wengineo.

Huna haja ya kuhofia kula ugali au wali, hasa ukiwa wa moto kwani ni fresh, salama na wenye ladha ya asili, na hakika utafurahia chakula. Hii inawafanya watalii wengi kutembelea mara nyingi na kufurahia muda wao wakiwa Tanzania.

Tanzania ndio nyumbani kwa Safari za ujasiri na kusisimua (Adventures)

Ndio. Uwepo wa mbuga za wanyama kama Serengeti, Mikumi, Manyara na Kilimanjaro, Tarangire, n.k ni sehemu ambazo utashuhudia moja kwa moja msisimo wa Adventures za wanyama na viumbe hai wengine wakipambana kuishi.

Utaona simba na chui wakiwinda, nyumbu wakihama eneo moja hadi lingine (Serengeti) pia Ngorongoro Crater yenye mifugo wa jamii za Kimasai na maajabu mengi zaidi ya aina za mimea na matunda, maua na kadhalika. Pia utapata fursa ya kupanda milima, kuendesha baiskeli, kuona maporomoko ya maji, kutembelea vijiji na kufanya mengine mengi kwenye nchi hii ya asili ya kutalii.

Saiti za kihistoria, ya mtu wa kale na mapango

Ukitaka kujua historia ya binadamu wa kwanza, ipo Tanzania. Olduvai Gorge, alama ya mguu wa mtu wa kale, mapango ya Pangani na yale yenye michoro ya Kondoa irangi, vyote vipo Tanzania. UNESCO imeweza kutunuku sehemu mbalimbali ikiwemo Kilwa na Mikindani kuwa World Heritage Sites.

Watu wakarimu wa kujumuika nao

Huenda umesikia au kuona kwenye televisheni kuwa Maasai ni watu wanaopenda kufuga, na mavazi yao ni ya kiafrika, na kudhania kuwa kama ni sanaa ya uigizaji. Kwa kila aliyefika na kutalii Tanzania, kashuhudia ukarimu huu wa ajabu. Wananchi wake wamekuwa na moyo wa pekee wa upole na ukarimu, kiasi cha kumkaribisha mgeni na kumhudumia kama vile ni mwenyeji. Hii imepelekea watalii kuhisi kuwa salama na huru kutembea maeneo mengi nchini, na pia kufanya mengi zaidi ya walivyopanga.

Kuthibitisha hili, Baraza la Dunia la utalii na usafiri limeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi salama zaidi duniani.